Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kuweka vikwazo vipya vya kiuchumi dhidi ya Iran, ambapo amesema nchi hiyo haitolipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi ya kijeshi.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumzia mashambulizi ya makombora katika kambi mbili za Marekani nchini Iraq, kwa kusema kuwa Marekani iko tayari kuendeleza amani, ingawa
ukweli ni kwamba ina jeshi kubwa na lenye vifaa imara.
Kwa mujibu wa Trump, amesema Iran inaonekana inajaribu kupunguza mvutano kati ya nchi hizo mbili ambao ulizidishwa makali na mauaji ya jenerali wa Iran, Qassem Soleimani aliyeuawa na Marekani wiki iliyopita.
Katika hotuba yake iliyosubiriwa kwa hamu, hapo jana Trump amesema hakuna mwanajeshi yeyote wa Marekani aliyejeruhiwa au kuuawa katika mashabulizi hayo ya jana.
Kuhusu mkataba wa nyuklia wa Iran, Trump amezitaka nchi washirika zilizobaki katika makubaliano hayo kujiondoa kama ambavyo Marekani ilifanya mwaka 2018.
Aidha, serikali ya Uingereza imekataa ombi la Rais Donald Trump wa Marekani la kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema makubaliano hayo yana umuhimu kwa London katika upande wa masuala ya kiusalama.
Mwisho.