Mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa unaendelea mjini New York huku viongozi wa dunia wakitoa mwito juhudi za haraka zifanyike kushughulikia ukosefu wa upatikanaji wa chakula wakati hofu ikiongezeka juu ya mavuno mabaya mwaka ujao kutokana na vita nchini Ukraine.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kuna dharura ya kutoa fedha kukabiliana na ukosefu wa upatikanaji wa chakula. Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amemkosoa rais wa Urusi Vladimir Putin kwa kuivamia Ukraine akisema hakuna amani kukiwa na njaa na haiwezekani kukabiliana na njaa bila amani. Rais wa Marekani Joe Biden atauhutubia mkutano huo hivi leo ambapo anatarajiwa kutangaza msaada mpya kwa Ukraine. Katika hotuba yake ya kwanza kwenye mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema nchi yake itafadhili usafirishaji wa ngano ya Ukraine kwenda Somalia inayokabiliwa na kitisho cha njaa.
CHANZO: DW SWAHILI