Jeshi la Nigeria limesema wanajeshi kumi na moja wameuawa katika shambulio lilifanyika katika jimbo la kati la Benue wakati wa operesheni ya kawaida.
Haya yanajiri wakati hali ya usalama ikiendelea kuzorota kote Nigeria na vikundi mbalimbali vyenye silaha vikianzisha vurugu.
Jeshi la Nigeria linasema kwamba askari hao, hapo awali walitangazwa kutoweka baada ya kuviziwa na watu wenye silaha.
Timu ya kuwatafuta na uokoaji baadaye iliwakuta wamefa siku ya Alhamisi katika eneo la Konshisha katika jimbo hilo.
Msemaji wa jeshi la Nigeria ameiambia BBC kwamba baadhi ya miili hiyo iliteketezwa. Alifafanua shambulio hilo kama uhalifu mbaya.
Kumekuwa na ripoti kwamba wanajeshi wamewafyatulia risasi kiholela raia kadhaa kujibu shambulio dhidi ya wanajeshi.
Jeshi la Nigeria limekanusha madai hayo. Bado haijafahamika ni nani aliyewauwa wanausalama na kwanini.
Lakini kama sehemu nyingi za Nigeria, jimbo la Benue limekuwa likikabiliwa na ghasia za kikabila, mapigano kati ya wafugaji na wakulima na shughuli za magenge ya wahalifu wenye silaha.