Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ajali ya boti katika Ziwa Kivu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imefikia 40, kufuatia kupatikana kwa maiti nyengine 27 jana Jumamosi.
Waziri wa mambo ya ndani, Basile Olongo, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba miili hiyo ilipatikana mpakani mwa kingo za mashariki za ziwa hilo upande wa nchi jirani ya Rwanda. Boti hiyo ilipinduka mwanzoni mwa wiki hii ikiwa imebeba watu takribani 200 na hadi sasa watu zaidi ya 100 hawajajulikana walipo. Rais Felix Tshisekedi aliitangaza Ijumaa kuwa siku ya maombolezo ya kitaifa. Ajali za vyombo vya majini zimekuwa jambo la kawaida katika mataifa mengi ya Maziwa Makuu, ambako vyombo kadhaa vya usafiri ni vikongwe na hujaza abiria kupita kiwango, huku vikiwa havina huduma za uokozi.
CHANZO: IDHAA YA KISWAHILI DW