Wafuasi wa mgombea wa upinzani wa Zambia Hakainde Hichilema wameanza kusherehekea wakati matokeo ya kwanza yaliyotolewa leo Jumamosi na tume ya uchaguzi yakionyesha kuwa kiongozi huyo wa upinzani anaongoza.
Matokeo ya kwanza yaliyotolewa na tume ya uchaguzi ya Zambia yanaonyesha kuwa kiongozi wa upinzani Hakainde Hichilema, amechukua uongozi wa mapema dhidi ya Rais aliyeko madarakani Edgar Lungu.
Tume ya uchaguzi ya Zambia imewahimiza watu kuwa watulivu wanaposubiri matokeo rasmi ya mwisho ili kuepuka machafuko.
Chini ya asilimia 20 ya kura zilizohesabiwa kati ya maeneo bunge 156, Hichilema anaongoza kwa kura 449,699 dhidi ya Rais Lungu mwenye kura 266,202.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Patrick Nshindano amesema matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa siku ya Jumatatu.
Wagombea 16 wa Urais waliwania wadhifa huo wakati wengine tayari wamekubali kushindwa na kumpongeza Hichilema kwa ushindi, wakinukuu matokeo yaliyotolewa hadi sasa katika vituo kadhaa vya kuhesabu kura.
#ChanzoDWSwahili