Maafisa wa polisi mjini Nakuru, Kenya wanamzuilia mwanamume anayedaiwa kuwauzia watu nyama ya paka.
Mwanamume huyo alikamatwa Jumapili ambapo inadaiwa alipatikana akimchuna ngozi paka. James Mukangi Kimani anadaiwa kuwauzia wauzaji wa samosa nyama hiyo, na pia kuuzia wenye migahawa.
Gazeti la Star linasema mwenyewe alikiri kupika samosa akitumia nyama hiyo.
Taarifa kwenye vyombo vya habari Kenya zinasema mwanamume huyo alikiri kuuza nyama ya paka zaidi ya elfu moja mjini humo tangu mwaka 2012.
Gazeti la Nation linasema aliwaambia wanahabari kwamba alianza 'biashara' hiyo baada ya "kugundua kulikuwa na pengo sokoni".
Alisema huwa anauza pia ngozi za paka na kwamba kwa kila paka hujipatia takriban Sh500 (Dola 5 za Marekani).
"Huwa nawaambia wateja wangu kwamba huwa naipata nyama hii kutoka Gioto (jaa la kutupa taka), lakini huwa hawajui kwamba ni nyama ya paka," alinukuliwa na gazeti la Nation.
Mwanamume huyo alifumaniwa eneo la Railways, Nakuru na alipigwa na umati wa watu kabla ya kuokolewa na maafisa wa polisi na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Ukulima.
Chini ya sheria za Kenya, ni haramu kula nyama ambayo haijakaguliwa na afisa wa afya ya umma, na pia kula nyama kutoka kwa mnyama ambaye haruhusiwi kuliwa Kenya.
Paka si miongoni mwa wanyama wanaoruhusiwa kuliwa chini ya Sheria za Kudhibiti Nyama Kenya. Mwanamume huyo anatarajiwa kufikishwa kortini leo Jumatatu.
Kwa hisani ya BBC
Picha na mtandao.