Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameonya utoaji taarifa za holela na upotoshwaji kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababisha na virusi vya corona (COVID 19) unaofanywa na watu mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa yote nchini, Makatibu Tawala wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Mikoa kwa njia ya video kutokea ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma.
Amezungumzia wajibu wa viongozi husika kuwa ni kushirikiana na mganga mkuu wa mkoa na wale wote walioko katika sekta ya tiba kuimarisha uratibu wa ugonjwa huu ndani ya mkoa.
Waziri Mkuu ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA ifuatilie watu wote wanaofanya upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Amewataka wakuu wa mikoa waimarishe utoaji wa elimu kwa umma ili wananchi waelewe athari za ugonjwa huo na namna ya kujikinga pamoja na kuwaondolea hofu waweze kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo.
Mwisho