Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo ametoa maagizo kwa wakuu wa wilaya,wakurugenzi na wakuu wa shule nchini,kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa usafiri kwa wanafunzi wote ambao wamekosa usafiri wa kurudi nyumbani mara baada ya shule zote kufungwa kufuatia uwepo wa ugonjwa Corona nchini.
Hii ni mara baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutoa tamko mnamo Machi 17,2020, la kufunga shule zote za awali, msingi na sekondari, vyuo vya kati pamoja na vyuo vikuu kwa siku 30 kutokana na tishio la ugonjwa wa Corona.
Waziri Jafo ametoa kauli hiyo leo Machi 20,2020 ofisini kwake jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa iwapo kuna shida inayowafanya wakuu wa shule washindwe kuweka utaratibu mzuri wa wanafunzi wote kurejea nyumbani wawasiliane na wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama ambao ni wakuu wa wilaya.
Aidha Mhe.Jafo ametoa pongezi kwa Mkuu wa Shule ya Kilakala iliyopo Morogoro na Mkuu wa Shule ya Dodoma Sekondari kwa kuweka utaratibu mzuri uliowezesha wanafunzi wote kurudi nyumbani hata kwa ambao wazazi wao hawakuwa na hela za nauli wameweza kufika bila ya shida yoyote.
Mwisho