Waziri mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev amewasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa rais Vladmir Putin leo.
Rais Putin alikutana na waziri Medvedev baada ya rais huyo kutoa hotuba yake kupitia televisheni ya taifa ambapo amependekeza kufanyia mageuzi katiba ili kulipa bunge uwezo wa kumteua waziri mkuu kwani katiba iliyopo kwasasa inampa rais mamlaka ya kumteua waziri mkuu.
Taarifa zinaeleza kuwa Medvedev alinukuliwa akisema kuwa katika muktadha huu ni wazi kwamba , baraza la mawaziri , linapaswa kumpatia rais wa nchi fursa hiyo ya kuchukua hatua zote zinazostahili.
Aidha, Rais Putin alinukuliwa akimuelekeza Medvedev kuendelea kuwa katika wadhifa wa waziri mkuu hadi pale baraza jipya la mawaziri litakapoundwa.
Katika hotuba yake kwa taifa Rais Putin alisema kuwa Medvedev atateuliwa kuwa naibu mkuu wa baraza la taifa la usalama nchini humo ambapo Putin ni mkuu wa baraza hilo.
Mwisho.