Watoto 26 wamekufa katika ajali ya moto uliounguza shule moja ya Kiislamu karibu na mji mkuu wa Liberia, Monrovia.
Ofisi ya rais wa nchi hiyo imesema hayo leo na kuongeza kwamba maafisa wa kutoa huduma za dharura wamemwambia Rais George Weah kwamba jumla ya watu 28, wamekufa kufuatia mkasa huo ambao umetokea usiku wa kuamkia leo. Afisa mmoja wa jamii ya Fulani Amadou Sherrif amesema moto ulitokea wakati watoto walikuwa wakilala. Msemaji wa ikulu Solo Kelgbeh amesema Rais Weah tayari amezuru eneo la Paynesville ilikotokea ajali hiyo ya moto. Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rais Weah ametuma rambirambi zake kwa familia ambazo zimewapoteza wapendwa wao. Ndugu na jamaa wamekusanyika nje ya lango kuu la jengo ambalo ndani yake kulikuwa na shule hiyo ya bweni ambayo paa lake limeteketea.
CHANZO: Idhaa ya Kiswahili DW