Maafisa wa usalama nchini Afrika Kusini hapo jana walikabiliana na waporaji kwa kutumia magurunedi na risasi za mpira katika juhudi za kutawanya makundi yaliokuwa yakilenga biashara zinazomilikiwa na raia wa kigeni nchini humo katika eneo la katikati mwa mji wa Johannesburg.
Mtu mmoja aliuawa na wengine watano kujeruhiwa. Ghasia hizo ni za punde zaidi za mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni mjini humo na maeneo mengine nchini humo. Takriban watu 10 wameuawa katika mashambulizi hayo ambayo pia yamechochea maandamano katika mataifa mengine barani Afrika. Baadaye kupitia ujumbe katika mtandao wa twitter, polisi wamesema kuwa hali hiyo imedhibitiwa. Msemaji wa polisi Xlolani Fihla amethibitisha kifo hicho kwa shirika la habari la AFP kufuatia ghasia hizo za jana ijapokuwa hakuweza kuthibitisha chanzo cha kifo hicho.
CHANZO: Idhaa ya Kiswahili DW