Watu sita wamefariki dunia na wengine kadhaa hawajulikani walipo, kufuatia mvua kubwa zilizosababisha maporomoko ya udongo katika wilaya ya Bududa mashariki mwa Uganda.
Shirika la Msalaba mwekundu la Uganda limesema karibu watu 50 wanaaminika kutojulikana walipo na nyumba 150 zimeharibiwa usiku wa Jumanne katika eneo la chini ya mlima Elgon. Shirika hilo limesema miongoni mwa waliokufa ni bibi wa miaka 73 na watoto watatu, na kuongeza kuwa watu wasiopungua 27 walijeruhiwa na karibu 350 wamelaazimika kuyapa kisogo makaazi yao. Limesema vifo zaidi vinatarajiwa mnamo wakati mvua zikiendelea kunyesha na uwezekano wa kuzuka kwa ugonjwa wa nemonia miongoni mwa watoto, na miripuko ya kipindupindu na kuharisha. Wilaya ya Bududa ilioko kwenye mpaka kati ya Uganda na Kenya, ni eneo la hatari kubwa ya kukumbwa na maporomoko ya udongo.
CHANZO: Idhaa ya Kiswahili DW