Star Tv

Serikali ya Shirikisho la Ujerumani kupitia Mpango wa Kusaidia Majeshi Rafiki imekubali kuongeza kipindi cha kutoa misaada kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa miaka 4 zaidi kuanzia mwaka 2021 hadi 2024 ambapo pamoja na mambo mengine itajenga Hospitali kubwa ya Kijeshi yenye kiwango cha “Level 4” Mkoani Dodoma

.

Balozi wa Ujerumani hapa nchini Mhe. Dkt. Detlef Wäechter akiwa na ujumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani ametangaza uamuzi huo leo tarehe 09 Mei, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Pamoja kujenga hospitali hiyo Mhe. Dkt. Wäechter amesema katika ushirikiano huo Ujerumani kupitia Timu ya Ushauri ya Wataalamu wa Kijeshi (GAFTAG) itaongeza mafunzo na vifaa vya ulinzi wa amani, itaendelea kufundisha madaktari wa Jeshi na kutoa vifaa vya matibabu na kutoa mafunzo ya ulinzi wa amani.

Katika ushirikiano wa sasa utakaoishia 2021, kati ya mwezi Juni 2017 na Machi 2019, Ujerumani imejenga Hospitali ya Kanda huko Monduli Mkoani Arusha ambayo imewekewa vifaa tiba vinavyotumia teknolojia ya kisasa na itakayotumiwa kama Hospitali ya Rufaa ikisaidiana na Hospitali ya Kijeshi ya Lugalo iliyopo Jijini Dar es Salaam. Ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu shilingi Bilioni 5 na Milioni 947 ambapo shilingi Milioni 346.8 kati yake zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Ufadhili mwingine uliotolewa ni upanuzi na uboreshaji wa Chuo cha Sayansi na Tiba cha Lugalo, ujenzi wa karakana za Jeshi katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga na Mwanza, ujenzi wa idara ya dharura ya Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika Hospitali ya Kanda iliyopo Bububu - Zanzibar, uboreshaji wa Hospitali za Kanda zilizopo Zanzibar, Mbeya, Mwanza na Tabora, msaada wa magari na vifaa tiba.

Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Ujerumani kwa kuendeleza na kuukuza uhusiano na ushirikiano na Tanzania na amemhakikishia Mhe. Balozi Wäechter kuwa Serikali ya Tanzania itahakikisha misaada yote inayotolewa inaleta manufaa yaliyokusudiwa.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Mabeyo na Katibu wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Bw. Malte Loknitz aliyeongoza ujumbe wa Maafisa kutoka Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani pamoja na Mshauri wa GAFTAG hapa nchini Luteni Kanali Thomas Nalbach.

 

CHANZO: Ikulu Mawasiliano Dar es Salaam 

Latest News

Mgogoro wa Maji unatishia Amani Duniani, inasema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa...
21 Mar 2024 14:18 - Kisali Shombe

Siku ya Maji Duniani ambayo inafanyika tarehe 22 Machi ikiwa na kaulimbiu: 'Maji kwa Ustawi na Amani. Ambapo maji ni moj [ ... ]

Matarajio katika mkutano wa BRICS nchini Afrika Kusini, Jumanne tarehe 22/2023
21 Aug 2023 12:14 - Kisali Shombe

Mkutano huo ambao utafanyikia Johannesburg nchini Afrika Kusini siku ya Jumanne, tarehe 22 Agosti 2023, unatarajiwa kuhu [ ... ]

Rais Ramaphosa Kuwa Mwenyeji wa Rais Xi Jinping wa China
21 Aug 2023 11:11 - Kisali Shombe

Rais Cyril Ramaphosa Jumanne ya tarehe 22 Agosti 2023, atakuwa mwenyeji wa Mheshimiwa Rais Xi Jinping wa China katika Zi [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2024 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.