Msemaji wa jeshi la Polisi nchini SACP David Misime amesema hali ya usalama na usimamizi wa ulinzi katika kampeni zinazoendelea nchini ni shwari na unaendelea vizuri.
Amesema Jeshi la Polisi limejiandaa vizuri katika kukabiliana na matishio ya aina yoyote ya kiusalama ambapo ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ya nchi ili kuhakikisha kampeni za uchaguzi mkuu zinafanyika kwa amani na utulivu.
Aidha, Kamanda Misime amewatahadharisha wananchi, viongozi wa kisiasa pamoja na wadau wengine wa uchaguzi kuendelea kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria za nchi.
Misime ametoa onyo kwa watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii na ikiwa itatokea baadhi ya watu wamefanya mambo yatakayopelekea uvunjifu wa amani na usalama wa nchi watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi la Polisi limesema liko imara kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama nchini inaendelea kuwa shwari hususani katika kipindi hiki ambacho kampeni zinaendelea, Ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza Uchaguzi Mkuu kufanyika siku ya Jumatano Octoba 28, 2020.