Star Tv

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza Mawaziri na Naibu Waziri wasimamie taasisi na idara zilizopo chini ya wizara zao ili zizingatie vigezo vyote vya utawala bora pamoja na kukemesha vitendo vya rushwa ambavyo ndio adui mkubwa wa utawala bora.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Ijumaa, Oktoba 29, 2021) wakati alipofungua Mafunzo ya Uongozi kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri katika Ukumbi wa Mtakatifu Gasper jijini Dodoma. Mafunzo hayo yameandaliwa na Taasisi ya Uongozi.

“Ninapenda kuwakumbusha kuwa ninyi ni nyenzo muhimu katika utendaji wa Serikali, hivyo wazembe, wezi na wabadhirifu waliopo chini ya mamlaka zenu lazima wote wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Serikali. Kila kiongozi lazima awe makini muda wote.”-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kupanua uelewa wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi ikiwa ni pamoja na kuelewa majukumu, madaraka na mipaka ya nafasi zao, kuongoza watu, kufanya maamuzi ya kimkakati na kuboresha sifa binafsi za kiuongozi.

Amesema ubadhirifu unatakiwa ushughulikiwe mapema kwa weledi na utaalam bila kulazimika kusimamisha utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa muda mrefu na hatua zichukuliwe bila kuoneana haya kama kuna ushahidi wa wazi kabla hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hajakagua au viongozi wa juu kuchukua hatua.

Amewataka viongozi hao kutumia mada zitakazowasilishwa ili ziweze kuwasaidia katika kuzisimamia vyema Wizara wanazoziongoza na taasisi zilizo chini ya wizara zao ”mwende mkazisaidie taasisi hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yake bila kikwazo chochote. Nendeni mkawe msaada kwao”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kwa kushirikiana na Taasisi zingine waendelee kusimamia amani na utulivu kwenye maeneo yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote. “Amani na utulivu ndiyo itatuwezesha kama nchi, tuendelee kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza mitaji yao hapa nchini.”

“Tunakumbushwa sisi viongozi wa Tanzania tuwe wazalendo na tuhakikishe tunaziendeleza rasilimali za nchi hii kwa faida ya Watanzania wote bila ubaguzi wa jinsia, kabila, dini na rangi ili mradi mtu hajavunja sheria. Tuwahudumie Watanzania wote kwa usawa.”

Pia, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi hao waepuke matumizi ya walinzi binafsi na waandishi wa habari binafsi katika Ofisi za Umma kwani wanaweza kuwa chanzo cha uvujaji wa siri za Serikali. “Upo utaratibu wa kufuata endapo itabainika mnahitajika kupatiwa wasaidizi hao. Zingatieni utaratibu huo na si vinginevyo.”

Latest News

Matarajio katika mkutano wa BRICS nchini Afrika Kusini, Jumanne tarehe 22/2023
21 Aug 2023 12:14 - Kisali Shombe

Mkutano huo ambao utafanyikia Johannesburg nchini Afrika Kusini siku ya Jumanne, tarehe 22 Agosti 2023, unatarajiwa kuhu [ ... ]

Rais Ramaphosa Kuwa Mwenyeji wa Rais Xi Jinping wa China
21 Aug 2023 11:11 - Kisali Shombe

Rais Cyril Ramaphosa Jumanne ya tarehe 22 Agosti 2023, atakuwa mwenyeji wa Mheshimiwa Rais Xi Jinping wa China katika Zi [ ... ]

Urusi Kuchagiza Maendeleo Afrika kupitia Nishati ya Nuklia na Madini ya Urani
12 Aug 2023 10:07 - Kisali Shombe

ROSATOM, taasisi ya nishati ya nyuklia ya serikali ya Urusi ambayo iliwaalika zaidi ya waandishi wa habari 15 kutoka nch [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2024 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.