Mgomo wa Mabasi uliotangazwa na Wamiliki wa Mabasi Tanzania TABOA kuafanyika leo Machi 10, kwa upande wa Mkoa wa Mwaza umezuiwa.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani ASP Joyce Kotecha akiongoza kikosi cha Usalama Barabarani katika kituo cha Mabasi yaendayo mikoani cha Nyabulogoya kilichoko Nyegezi Wilayani Nyamagana amewataka Wamiliki wa Mabasi pamoja na Madereva kusitisha mgomo na kuendelea na safari kama kawaida.
ASP Kotecha amemewaambia Wamiliki hao wanapaswa kusitisha mgomo huo kwa kuwapatia elimu juu ya athari zitakazowapata kama watafanya mgomo ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni ya usafirishaji, ndipo Mabasi katika Stendi ya Nyabulogoya yakaanza safari na kuamua kusitisha mgomo uliokuwa ufanyike.
Machi 6, 2021 Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), kiliitisha kikao cha dharura cha kusimamisha huduma ya kusafirisha abiria endapo suala la kutumia mashine za kukatia tiketi kwa njia ya mtandao POS halitapatiwa ufumbuzi.
Mashine za POS zinamtaka mmiliki wa fedha kuweka kiasi cha fedha katika laini ya simu au wakala wa huduma za fedha kwa makadirio ya abiria wa basi husika, suala ambalo wamiliki wanasema lina gharama kubwa kuliko faida.
Kutokana na kikao hicho cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania TABOA asimilia kubwa ya wajumbe wa mkutano huo waliazimia kuegesha mabasi yao leo Machi 10, 2021 endapo suala hilo halitashughulikiwa.