Makamu wa Kwanza wa Rais visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amefariki dunia.
Habari hizo zimethibitishwa leo na Rais wa Zanzibar, Dokta Hussein Ali Hussein Mwinyi wakati akizungumza na waandishi wa habari visiwani humo.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Maalim amefariki Dunia majira ya saa tano asubuhi leo Februari 17,2021.
Amesema Makamu huyo wa Rais amefariki katika hospitali ya Muhimbili ambapo alipokuwa amelazwa akipatiwa matibabu tangu Februari 09,2021.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa pole pamoja na salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, Watanzania, pamoja na Chama cha ACT Wazalendo kufuatia msiba huo.
Aidha, Rais Mwinyi ametangaza siku saba za maombolezo ambapo amesema bendera zitapepea nusu mlingoti, Na kusema taarifa zaidi za msiba huo zitaendelea kutolewa kadiri itakavyowezekana kupitia serikali kwa kushirikiana na familia yake pamoja na Chama cha ACT Wazalendo.
Maalim Seif Sharif amefariki dunia akiwa ametumikia wadhifa wa makamu wa kwanza wa rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa chini ya siku 100, akiwa sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa baada ya Uchaguzi Mkuu 2020.