Polisi jijini Dar es Salaam wameeleza sababu za kumshikilia Askofu Emmaus Mwamakula wa Kanisa la Uamsho la Morovian.
Askofu Emmaus Mwamakula anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhamasisha wananchi nchi nzima kufanya maandamano ya kudai katiba mpya.
Kwa mujibu wa mkuu wa kanda maalumu ya polisi jijini Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema Askofu Mwamakula ameitisha maandamano hayo kupitia mitandao ya kijamii bila kuomba kibali cha polisi.
Maandamano hayo yalipangwa kuaanze leo Februari 16.
"Tulitegemea Askofu wa Moravian Uamsho ambaye ni kiongozi wa kiroho angewahubiria wananchi kufuata sheria lakini tulipoona Dkt Mwamakula anahamasisha watu waingie Barabarani kudai tume huru ya uchaguzi na katiba na kuhamasisha vurugu ikabidi tumkamate"- Kamanda Mambosasa wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Kupitia mitandao yake ya kijamii Askofu Mwamakula amekuwa akihamasisha wananchi kuungana naye katika matembezi ya hiyari yenye lengo la kudai Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa Askofu huyo, alibainisha matambezi hayo ya amani yangefanyika kwa awamu, awali ya kwanza ni jijini Dar es Salaam na kisha yatahamia mikoani.
Kamanda Mambosasa pia amesema Askofu huyo amekamatwa kwa mahojiano kwa kuwa taarifa yake ilileta taharuki kwa umma kupitia mitandao ya kijamii.