Marekani imeidhinisha chanjo aina ya Moderna kama chanjo ya pili ya corona nchini humo, baada idhini ya kusambazwa kwa dozi za chanjo hiyo kutolewa.
Mamlaka ya kusimamia usalama wa chakula na dawa (FDA) iliidhinisha chanjo hiyo iliyongenezwa Marekani karibu wiki moja iliyopita baada ya kuidhinisha chanjo ya Pfizer/BioNTech ambayo kwasasa inatolewa.
Marekani ilikubali kununua dozi milioni 200 ya Moderna, na milioni sita kati ya hizo huenda ziko tayari kusafirishwa.
Kamishna wa FDA Stephen Hahn amesema kuidhinishwa kwa dharura kwa chanjo hiyo siku ya Ijumaa kunaashiria ''hatua nyingine muhimu katika juhudi za kukabiliana na janga la kimataifa ".
Hatua ya kuidhinishwa kwa chanjo hiyo ilifikiwa baada ya jopo la wataalamu kupiga kura siku ya Alhamisi 20-0 huku wito ukitolewa kwamba ubora wa chanjo ya Moderna unazidi madhara yake kwa watu waliyo na umri 18 na zaidi.
Wadhibiti waliripoti mapema wiki hii kwamba chanjo ya Moderna ilikuwa salama na inafanya kazi kwa asilimia 94.
Rais wa Marekani Donald Trump,aliandika katika mtandao wake wa Twitter saa kadhaa kabla ya tangazo rasmi kutolewa alisema chanjo hiyo "imeidhinishwa kwa kishindo" na itaanza kusambazwa "mara moja”.
Huku Rais mteule Joe Biden, ambaye anajiandaa kupewa chanjo siku ya Jumatatu, amesema kuidhinishwa kwa chanjo za sindano za Pfizer na Moderna "kunatuhakikishia siku njema huko mbele".