Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema maafisa wa Umoja wa Mataifa watapewa kibali cha kuzuru na kukagua kinu na kambi ya nyuklia ya Zaporizhzhia.
Ikulu ya Kremlin imetoa tangazo hilo baada ya mazungumzo kwa njia ya simu kati ya Putin na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Hatua hiyo inakuja huku madai ya mapigano karibu na mtambo huo yakiendelea, na kusababisha raia wanne kujeruhiwa na makombora ya Urusi.
Mbali na hilo, Marekani hapo jana siku ya Ijumaa imeahidi kutuma silaha na risasi zaidi kusaidia katika juhudi za vita vya Ukraine.
Kufuatia mazungumzo ya viongozi hao wa Ufaransa na Urusi, Kremlin ilisema, Putin amekubali kuwapa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa "msaada unaohitajika" ili kufikia eneo la nyuklia la Zaporizhzhia.
Kinu hicho kimekuwa chini ya umiliki wa Warusi tangu mapema Machi lakini mafundi wa Kiukreni bado wanakiendesha chini ya maelekezo ya Urusi.