Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limepinga vikali sheria mpya iliyopitishwa na bunge la Denmark ambayo itairuhusu nchi hiyo kushughulikia madai ya wakimbizi wanaoomba hifadhi nje ya bara la Ulaya.
Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi, amesema katika taarifa ya jana usiku kwamba ikiwa sheria hiyo itaanza kutumika, basi itapelekea wakimbizi wanaoomba hifadhi kuhamishwa kwa nguvu, na Denmark itaweza kukwepa jukumu lake la kuwapa hifadhi wakimbizi wanaoishi katika mazingira magumu. Denmark ni taifa lenye misimamo mikali katika suala la uhamiaji, na inakusudia kupokea tu wakimbizi chini ya mfumo wa Umoja wa Mataifa wa kugawana wakimbizi kati ya mataifa ya Ulaya.
CHANZO: IDHAA YA KISWAHILI (DW).