Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amezituhumu nchi za Magharibi kwa kujaribu kutumia tukio la kulazimishwa kutua mjini Minsk ndege ya Ryanair mwishoni mwa wiki ili kuanzisha vita vya kisiasa dhidi yake na kusema zimetumia uwongo kueleza jinsi alivyolishughulikia tukio hilo.
Katika matamshi yake ya kwanza baada ya baadhi ya wanasiasa wa Ulaya kuliita tukio hilo la Jumapili kuwa ni "utekaji nyara uliofadhiliwa na serikali", Lukashenko ameliambia bunge kuwa alichukua hatua halali na kwa mujibu wa sheria zote za kimataifa, lakini watu wenye nia mbaya wanajaribu kutumia tukio hilo la ndege kuhujumu utawala wake. Belarus ilitumia kisa hicho kumkamata mwandishi wa habari wa siasa za upinzani aliyekuwemo ndani ya ndege hiyo Raman Pratasevich. Kiongozi wa upinzani aliyeko uhamishoni Sviatlana Tsikhanouvskaya amesema leo kuwa upinzani unajiandaa kwa awamu mpya ya maandamano ya kuipinga serikali nchini Belarus.
CHANZO:
IDHAA YA KISWAHILI (DW)