Star Tv

Takriban watu 44 wamekufa baada ya kukanyagana kwenye tamasha la kidini lililohudhuriwa na maelfu ya waumini wa Kiyahudi wa madhehebu ya Othordox kwenye eneo la Kaskazini mwa Israel na kuwajeruhi wengine zaidi ya 150.

Tukio hilo limetokea mapema leo asubuhi Aprili 30 baada ya mahujaji waliokuwa wamekusanyika kwenye eneo la Mlima Meron ambako kuna kaburi mashuhuri la Rabbi Shimon Bar Yochai, ambapo waumini hao walikuwa wakiadhimisha sikukuu ya kidini ya Lag BaOmer.

Ajali hiyo imeelezwa kuwa moja ya matukio mabaya kwa raia kuwahi kushuhudiwa nchini Israel.

Vyombo vya habari vimekadiria kuwa takriban watu 100,000 walikuwepo kwenye eneo hilo.

Shimon Lavi, Kamanda wa polisi Kaskazini mwa Israel, amesema tukio hilo ni la kusikitisha na kwamba polisi walifanya kila waliloweza kuokoa maisha ya watu na kusaidia kuwapeleka hospitali.

Msemaji wa Magen idara inayohusika na shughuli za uokozi, David Adom amesema kulikuwa na watu 38 waliokufa katika eneo la tukio, lakini wengine zaidi walifia hospitali.

Idara hiyo ya uokozi imesema ilikuwa inawahudumia watu 150 waliojeruhiwa, sita kati yao wakiwa katika hali mbaya.

Wizara ya Sheria imesema idara ya upelezi wa ndani ya polisi imeanzisha uchunguzi wa ajali hiyo, kuangalia iwapo kuna uwezekano wa kuwepo uzembe au kutowajibika ipasavyo kwa maafisa wa polisi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewasili kwenye eneo la tukio. Netanyahu amelielezea tukio hilo kuwa ni maafa makubwa na kusema kuwa kila mmoja anawaombea wahanga.

Naye Rais wa Israel, Reuven Rivlin ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba anaifutailia hali inavyoendelea huko Meron na anawaombea majeruhi wapone haraka.

Salamu za pole zimekuwa zikitolewa na viongozi mbalimbali ulimwenguni kutokana na mkasa huo, akiwemo Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas.

Sherehe hizo ziliahirishwa mwaka jana kutokana na janga la virusi vya corona, hivyo mkusanyiko huo ulikuwa wa kwanza kuwakutanisha maelfu ya watu nchini Israel tangu kuondolewa kwa vizuizi vya kuzuia kuenea kwa virusi hivyo na baadhi ya watu kupata chanjo ya COVID-19.

 

Latest News

“TUTAJIRIDHISHA KABLA YA KUKUBALI CHANJO YA CORONA”- Rais Samia.
14 May 2021 18:24 - Grace Melleor

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kabla ya kupokea chanjo ya virusi vya Corona ni lazi [ ... ]

SOMALIA YATANGAZA KUREJESHA UHUSIANO NA KENYA.
06 May 2021 17:57 - Grace Melleor

Somalia imetangaza kuwa inarejesha mahusiano ya kidiplomasia na nchi jirani ya Kenya baada ya kusitisha mahusiano hayo m [ ... ]

KENYA NA TANZANIA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA.
05 May 2021 15:39 - Grace Melleor


Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania iko tayari kuwapokea wawekezaji kutoka Kenya pamoja na kuondoa vikwazo visivy  [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2021 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.