Mwana Mfalme Hamzah Al-Hussein wa Jordan ambaye anaripotiwa kushikiliwa kwenye kifungo cha nyumbani, amesema atakaidi amri ya jeshi iliyomtaka akae kimya.
Sauti ya Mwana Mfalme huyo iliyotumwa mtandaoni inaelezea kwamba hatakubali kuzuiwa kutoka nje, kutuma ujumbe kwenye ukurasa wa Twitter na ama kuwasiliana na watu wengine.
Ndugu huyo wa baba mmoja wa Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan aliripoti kuzuiliwa tangu jana, huku serikali ikisema imezuia jaribio la mapinduzi, ingawa haikumtaja Hamzah kuhusika na jaribio hilo.
Mama yake ambaye ni Malkia Noor, alisema mwanae na wenzake wengine wanaoshikiliwa ni waathirika wa kile alichokiita kuwa ni fitina ovu.
Mwana Mfalme Hamzah ndiye aliyekuwa awe Mrithi wa kiti cha Ufalme kwa mujibu wa wosia wa baba yao Mfalme Hussein, lakini baadaye Mfalme Abdullah alimuondowa kwenye nafasi hiyo na kumuweka mwanae wa kwanza wa kiume, Hussein al-Hussein.