Takribani watu 180 wamekwama ndani ya hoteli moja kwenye mji wa kaskazini mwa Msumbiji, baada ya kuzingirwa na wanamgambo kwa zaidi ya siku tatu, huku watu kadhaa wakiripotiwa kufa.
Wanamgambo wa jihadi walianzisha mashambulizi siku ya Jumatano mchana na kuwalazimisha wakaazi kukimbilia msituni.
Kwa mujibu wa mashirika ya haki za binaadamu na watu walioshuhudia, shambulizi hilo limetokea kwenye eneo la Palma karibu na eneo lenye mradi mkubwa wa gesi asilia kwenye jimbo la Cabo Delgado.
Mashambulizi hayo yalitokea baada ya kampuni kubwa ya mafuta ya Ufaransa, Total kutangaza kwamba kazi itaanza tena, Kampuni ya Total ni mwekezaji mkubwa katika mradi wa mafuta kwenye jimbo hilo, huku kukiwa na kampuni sita za kimataifa ikiwemo ExxonMobil.
Serikali ya Msumbiji imesema miongoni mwa watu waliozingirwa katika Hoteli ya Amarula ni pamoja na wafanyakazi wa kimataifa na vikosi vya usalama na kwamba operesheni za kuwaokoa zinaendelea.
Mfanyakazi mmoja wa kampuni ya LNG amesema takriban mji wote umeharibiwa na watu wengi wameuawa. Hata hivyo hakufafanua zaidi kuhusu watu waliouawa wala uraia wao.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Human Rights Watch limesema washambuliaji wana mafungamano na kundi la Msumbiji la Al-Shabaab, ambalo lakini halina uhusiano wa moja kwa moja na kundi la jihadi la Somalia lenye jina kama hilo.
Watu kadhaa walioshuhudia wameiambia Human Rights Watch kwamba waliona miili ikiwa mitaani na wakaazi wakikimbia baada ya wapiganaji wa Al-Shabaab kuwafyatulia risasi watu na majengo.
Serikali ya Msumbiji imethibitisha kutokea kwa shambulizi hilo na imesema wanajeshi wameanzisha operesheni ya kupambana na wapiganaji kwenye mji huo.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi, Kanali Omar Saranga amesema vikosi vya ulinzi na usalama vinafanya kazi usiku na mchana kurejsha usalama haraka iwezekanavyo kwa watu wa eneo hilo pamoja na miradi ya kiuchumi karibu na eneo hilo.
Taarifa iliyotolewa Ijumaa na Ubalozi wa Marekani mjini Maputo, imelaani vikali shambulizi hilo la Palma na umeahidi kushirikiana na serikali ya Msumbiji kupambana na ugaidi.