Rais wa Marekani Joe Biden amesema Vladimir Putin atajuta kwa juhudi zake za kujaribu kushawishi uchaguzi wa urais wa mwaka wa 2020 nchini Marekani kwa niaba ya Donald Trump.
Ripoti ya ujasusi ya Marekani iliyotolewa Jumanne wiki hii inaunga mkono shutuma za muda mrefu kwamba baadhi ya maafisa wa jeshi wa Donald Trump walishirikiana na Urusi kwa kuongeza mashtaka kutoka kwa maafisa wa Ukraine wenye uhusiano wa karibu na Moscow dhidi ya mpinzani wa wakati huo Joe Biden kutoka chama cha Democratic, kabla ya uchaguzi wa mwezi Novemba 2020.
Kwa upande wake Urusi imesema madai hayo hayana msingi wowote na kuyaeleza madai ya idara za upelelezi za Marekani kuwa siyo ya kweli.
Ripoti ya ujasusi ya Marekani iliyotolewa imeongeza maelezo mengine kwenye tuhuma kuwa baadhi ya maafisa waandamizi wa Trump walijaribu kushirikiana na Urusi kwa kusisitiza madai yaliyotolewa dhidi ya aliyekuwa wakati huo mgombea Joe Biden na viongozi wa Ukraine wenye mahusiano na Urusi kuelekea uchaguzi wa Novemba 3.
Ubalozi wa Urusi nchini Marekani umesema katika taarifa kuwa waraka uliotayarishwa na idara ya ujasusi ya Marekani ni tuhuma nyingine zisizo na msingi dhidi ya Urusi kwa kuingilia michakato ya kisiasa ya ndani ya Marekani.
Imesema hakuna maelezo na ushahidi uliotolewa kuthibitisha tuhuma hizo.
Duru tatu zimesema kuwa Marekani inatarajiwa kuiwekea vikwazo Urusi katika siku chache zijazo kwa sababu ya tuhuma hizo.