Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan amejitosa tena kuwania kurejea madarakani katika uchaguzi wa mwaka ujao baada ya kuhama chama cha siasa, Ambapo amejiunga na chama tawala cha All Progressives Congress (APC) ambacho kilimshinda mwaka 2015 baada ya kukaa madarakani kwa miaka mitano.
Kundi la wafuasi lilinunua fomu ya uteuzi kwa niaba yake siku ya Jumatatu, na kuendeleza mtindo wa wanaotaka kutumia washirika kununua fomu hiyo.
Uamuzi wake wa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuwania urais akiwa na chama cha APC umewashangaza sana Wanigeria wengi, hasa wale wa chama chake cha zamani, People’s Democratic Party (PDP).
Kwa muda wa miezi kadhaa, uvumi ulikuwa umezagaa kuhusu kujihusisha kwake kwa siri katika chama tawala lakini si Bw Jonathan wala washirika wake walikuwa wametoa maoni yao.
Haijabainika kwa nini Jonathan aliamua kubadili vyama, lakini kumekuwa na fununu kwamba amekuwa hana furaha kufuatia kushindwa kwake kwenye uchaguzi wa 2015, ambapo inasemekana alihisi kusalitiwa na washirika wakuu ndani ya chama.
Anastahiki muhula mmoja zaidi iwapo atashinda katika uchaguzi wa mwaka ujao jambo ambalo linaweza kumaanisha mamlaka kurejea katika eneo la kaskazini mwa Nigeria katika mpangilio ambao haujaandikwa, wenye utata ambao unabadilisha mamlaka kati ya kaskazini na kusini.