Hospitali moja ya binafsi jijini Nairobi imesitisha utoaji chanjo ya Covid-19 kutokana na uhaba wake, licha ya serikali kuwa na zaidi ya dozi Milioni moja.
Hospitali ya Aga Khan ilitangaza kwamba itaendelea na huduma za utoaji chanjo wakati itakapopata chanjo zaidi kutoka kwa serikali.
Wizara ya Afya siku ya Jumanne ilisema ni watu 130,575 pekee ambao wamechanjwa kote nchini kufikia sasa, licha ya dozi 806,000 kusambazwa kati ya dozi Milioni 1.12 zilizopo.
Hayo yanajiri baada ya hospitali nyingine ya kibinafsi kuanza kutoza ada ya kupata chanjo ya corona ya Sputnik V ya Urusi, ambayo serikali imetoa tahadhari dhidi ya utumiaji na usambazaji wake.
Serikali ya Kenya imeidhinisha matumizi ya chanjo ya Oxford-AstraZeneca.
Ubalozi wa Urusi nchini Kenya siku ya Jumatatu ilijitenga na uingizaji wa chanjo ya Sputnik V nchini humo.