Waziri anayesimamia maafisa wa polisi Bwana Bheki Cele ameionya migahawa ya Afrika Kusini kuacha kuuza pombe kwa kutumia vikombe vya chai
Waziri Bheki ametoa onyo hilo mara baada ya katazo la watu kunywa pombe nchini humo kutolewa kutokana na ongezeko kubwa maambukizi ya virusi vya corona.
Waziri huyo ameionya migahawa dhidi ya kuficha ukweli kwa kutumia vikombe vya kunywa chai kuwekea pombe wakati huu ambapo uuzaji wa pombe umepigwa tena marufuku.
Rais Cyril Ramaphosa amesema "tabia mbovu" zinazosababishwa na unywaji wa pombe ndio chanzo cha kuongezeka kwa usambaaji wa virusi vya corona wakati anatangaza marufuku hiyo Jumatatu.
Mlipuko mpya wa virusi vya corona unaosambaa kwa kasi ya juu nchini Afrika Kusini umeshuhudiwa nchini humo kwa kipindi cha wiki mbili za hivi karibuni.
Pia amepiga marufuku mikusanyiko wakati wa mazishi, saa za kutoka nje ni kuanzia saa tatu usiku hadi kumi na mbili asubuhi, na kuagiza maduka yote, baa na maeneo mengine kufungwa kufikia saa mbili usiku.
Waziri Bheki Cele ameonya migahawa dhidi ya kutumia mbinu za kijanja za kunywa pombe kupitia vikombe vya chai iliyopigwa marufuku
Akizungumza katika mkutano na wanahabari,waziri Bheki Cele alisema migahawa itakayokiuka agizo hilo itapoteza leseni na wamiliki kushtakiwa.
"Msiweke pombe kwenye vikombe vya kunywa chai migahawani. Musiweke pombe kwenye chumba za vinywaji zilizoandikwa kinywaji hiki hakina pombe kabisa. Tunajua ujanja munaotumia,.. Ikiwa tutaona kuna kitu tofauti kwenye vikombe vya kunywa chai - tutahakikisha mnapoteza leseni zenu"-Bwana Cele amesema.
Inasemekana kwamba kuna baadhi ya migahawa ambayo imekuwa ikitumia mbinu janja kuuza pombe licha ya kupigwa marufuku hiyo ambayo itaendelea kutekelezwa hadi katikati ya Januari.