Kenya imerekodi viwango vya juu vya maambukizi ya virusi vya corona kwa siku baada ya wagonjwa wapya 45 kuthibitishwa leo na kufikisha idadi ya watu 535 waliopatikana na ugonjwa wa Covid -19.
Waziri Kagwe amesema wagonjwa hao wamepatikana baada ya sampuli 1,077 kufanyiwa uchunguzi katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Wagonjwa 29 wote walithibitishwa kuwa wa Nairobi na wanatokea mtaa wa Eastleigh, huku wengine 11 wakiwa ni wa Mombasa na wangine watano wakitokea Wajiri Kaskazini mwa Kenya.
Wizara hiyo pia imetangaza kuwa wagonjwa tisa ambao walikuwa wameambukizwa ugonjwa huo wamepona na kufanya idadi ya waliopona kufikia 182 watu waliopona kutokana na maradhi hayo.
Katika juhudi za kudhibiti maambukizi hayo Kenya bado inaendeleza marufuku ya watu kutotoka nje kuanzia saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri.
Marufuku ya usafiri kuingia na kutoka mji kuu wa Nairobi na miji mingine kama vile Madera ,Mombasa, Kilifi na Kwale pwani ya Kenya pia iliwekwa kukabiliana na maambukizi.
Hivi karibuni Wizara ya Afya iliweka masharti mapya ya uendeshaji Migahawa Kenya, ambapo ilisema kuwa itaruhusu Migahawa kuanza kufunguliwa kuanzia saa 11 asubuhi na kufungwa saa 10 jioni.