Wananchi wa Kenya wanaendelea kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Daniel Arap Moi, aliyefariki dunia wiki iliyopita ambapo leo ni siku ya tatu na ya mwisho tangu wananchi wa Kenya waanze kutoa heshima kwa kiongozi wao.
Mwili wa kiongozi huyo aliyeongoza Kenya kwa miaka 24, umekuwa ukiagwa katika majengo ya bunge jijini Nairobi kwa siku mbili zilizopita, na leo nafasi imetolewa kwa wananchi wa kawaida kumuaga kiongozi wao.
Shughuli ya kuuaga mwili huo ilianza Jumamosi Februari 8 na kutarajiwa kumalizika leo Jumatatu. Siku ya Jumanne ambapo kutafanyika misa ya wafu katika uwanja wa kimataifa wa Moi.
Mazishi ya kiongozi huyo wa zamani, yatafanyika siku ya Jumatano nyumbani kwake huko Kabarak katika kaunti ya Nakuru lakini kesho, kutakuwa na ibada ya kitaifa katika uwanja wa Nyayo, inayotarajiwa kuhudhuriwa pia na marais mbalimbali kutoka barani Afrika.
Mwisho.