Mahakama ya Juu Kenya kutoa uamuzi kuhusu uchaguzi wa rais Kenya Mahakama ya juu nchini Kenya itatoa uamuzi wake leo wa kama itaidhinisha au kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwezi uliopita.
Mahakama hiyo yenye majaji saba itatoa uamuzi baada ya wiki iliyopita kusikiliza kwa siku tatu hoja za mawakili wanaowasimamia wagombea wawili wakuu na makundi pinzani ya makamishena wa tume ya uchaguzi. William Ruto, ambaye alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo wa Agosti 9, amesema jana kuwa ataheshimu uamuzi wa Mahakama ya Juu kwa sababu Kenya ni nchi inayofuata utawala wa kisheria. Ruto ambaye ni naibu wa rais, alitangazwa mshindi na tume ya uchaguzi kwa kupata asilimia 50.49 dhidi ya asilimia 48.85 ya kiongozi mkongwe Raila Odinga aliyeungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta. Odinga alipinga matokeo hayo na kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Upeo akidai kulikuwa na udanganyifu katika mchakato wa kuhesabu kura. Mgombea mwenza wa Odinga, Martha Karua alisema muungano wao wa Azimio One Kenya pia utaheshimu uamuzi wa leo.
CHANZO: DW SWAHILI