Kamishna Mkuu wa Uingereza Jane Marriott ametupilia mbali madai kwamba yeye na nchi yake waliingilia uchaguzi mkuu wa Kenya uliomalizika hivi majuzi.
Marriott alikuwa akijibu madai kwenye mitandao ya kijamii kwamba aliishinikiza tume ya uchaguzi kumtangaza William Ruto kuwa rais mteule baada ya uchaguzi huo.
Baadhi ya watumiaji wa mtandao waliweka picha mtandaoni ambazo hazijathibitishwa zikionesha Marriot akisalimiana na Ruto na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati.
Katika mfululizo wa jumbe za twitter, Marriott amesema Uingereza "haiungi mkono wala haina maoni yoyote juu ya wagombeaji au vyama vyovyote katika uchaguzi", na kuyataja madai hayo kuwa "habari potofu".
“Ni nani Wakenya wanamchagua ni suala la watu wa Kenya. Tulikutana na watu kutoka katika nyanja mbalimbali za kisiasa ili kueleza mipango na ushirikiano wa Uingereza na Kenya, ikiwa ni pamoja na taasisi huru,”-Amesema Marriott.
Aidha Marriott amesema Kenya itasalia kuwa mshirika muhimu wa Uingereza, akiongeza kuwa Uingereza iko tayari kuunga mkono viongozi waliochaguliwa na wananchi.
#ChanzoBBC