Kiongozi wa upinzani nchini Belarus Maria Kolesnikova amechana paspoti yake ili kuzuia asifukuzwe nchini humo.
Hali hiyo imetokea wakati maafisa nchini Belarus walipojaribu kumuondoa nchini humo kwa nguvu kiongozi huyo lakini alichukua uamuzi wa kuchana hati yake ya kusafiria akipinga hatua hiyo na kuruka kutoka katika gari aliyokuwemo ndani.
Kolesnikova ambaye ni mmoja wa viongozi wa mwisho ambao bado wako nchini humo wakiongoza maandamano dhidi ya rais Alexander Lukashenko, alikamatwa mpakani baada ya kutoonekana siku ya Jumatatu.
Maafisa wa mpakani wamesema alikuwa anajaribu kutoroka nchini humo lakini wenzake wawili aliokuwa nao ambao waliingia nchini Ukraine wamesema aligoma kufukuzwa nchini humo.
Katika mkutano na waandishi habari kwenye mji mkuu wa Ukraine Kiev, Katibu wa habari wa baraza la uratibu la upinzani, Anton Rodnenkov , pamoja na Katibu wake Mkuu Ivan Kravtsov walielezea kuhusu matukio kadhaa wakati watu hao watatu wakipelekwa mpakani.
CHANZO:DW Swahili.