Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha moto uliotokea usiku wa jana Julai 10, katika Soko Kuu la Kariakoo lililopo jijini Dar es Saalam.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo Julai 11, 2021 na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Samia amesema Soko la Kariakoo licha ya kuajiri wafanyabiashara wengi lakini ni kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki hivyo tukio hilo si hasara kwa Wafanyabiashara tu bali hata kwa Serikali.
Aidha, Rais Samia ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala na wafanyabiashara wa soko hilo kufuatia hasara kubwa waliyoipata kutokana na ajali ya moto huo.
Katika upande mwingine Rais Samia pia ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martin Shigella na Jumuiya za Kiislamu Tanzania kufuatia kuungua moto kwa Bweni la Shule ya Sekondari ya Kiislam ya Wasichana AT TOWN inayomilikiwa na Taasisi ya Kiislamu iliyopo mji Mpya katika Manispaa ya Morogoro.
Rais Samia ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na jumuiya za dini nchini kutafuta vyanzo vya matukio hayo na kuweza kuyadhibiti matukio hayo yasijirudie kwa kuwa kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya kuungua moto kwa shule zinazomilikiwa na jumuiya hizo hap nchini.