Kiongozi wa chama cha ODM nchini Kenya Raila Odinga ameruhusiwa kutoka hospitalini na sasa anaendelea kupata afueni nyumbani kwake Karen mjini Nairobi.
Raila Odinga alituma video kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akifanya mazoezi ya viungo, huku akiwa anasema "Nafurahi nimerejea nyumbani".
Raila alisema kwamba amethibitishwa kupatikana na virusi vya corona Alhamisi, na kusihi raia kuendeleza kanuni za kukabiliana na virusi hivyo.
Raila mwenye umri wa miaka 76 alithibitisha kwamba amefanyiwa vipimo katika hospitali ya Nairobi baada ya kulalamika kwamba ana uchovu aliporejea Nairobi kutoka kampeini za siku tano katika eneo la Pwani alipokuwa anafanya kampeni kwa ajili ya ripoti ya BBI.
Daktari wa Raila Dkt. David Oluoch Olunya, Alhamisi alisema kuwa kiongozi huyo wa ODM anapokea matibabu na wanazidi kuifuatilia kwa makini hali yake.
Kiongozi huyo wa chama cha (ODM) alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Nairobi.