Uchunguzi umeanzishwa nchini Ufaransa baada ya kutoweka kwa mwanafunzi Msenegali mwenye kipaji ambaye alikuwa akisoma katika shule ya kifahari mjini Paris.
Mwanafunzi huyo Diary Sow hakurejea shuleni baada ya mapumziko ya Krismasi na kusababisha hofu Senegal na Ufaransa.
Akielezewa kama "mwanafunzi bora wa Senegal", Bi Sow alishinda tuzo kadhaa za kielimu na kuchapisha kitabu chake cha kwanza cha tamthilia mwaka jana.
Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 20, hajaonekana tangu tarehe 4 Januari.
Raia wa Senegal wanaoishi katika mataifa ya kigeni wamekuwa wakimtafuta kupitia mitandao ya kijamii.
Huku watu mashuhuri wa Ufaransa ikiwa ni pamoja na mcheza filamu Omar Sy, wameshirikisha umma ombi lao la kutafutwa kwa Bi Sow kupitia mitandao ya Instagram na Twitter.