Israel itafanya uchaguzi wake wa nne katika kipindi cha miaka miwili baada ya vyama vikuu viwili katika serikali ya umoja kushindwa kuheshimu muda wa mwisho wa kutatua mzozo juu ya bajeti ya taifa.
Israel imeitisha uchaguzi huo mwezi Machi baada ya bunge kushindwa hapo jana kuidhinisha bajeti ya serikali ikiwa ndiyo muda wa mwisho uliopangwa kufanya hivyo.
Kampeni za uchaguzi wa nne wa bunge ndani ya miaka miwili, zitafanyika wakati Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akiwa anakabiliwa na changamoto kadhaa.
Miongoni mwao ni hasira ya umma inayotokana na jinsi alivyoshindwa kukabiliana na janga la virusi vya corona, huku akiwa katikati ya kesi ya ufisadi, ya kwanza dhidi ya waziri mkuu wa Israel.
Mpinzani mkuu wa Netanyahu katika uchaguzi ujao ni Gideon Saar, mwanasiasa aliyejitenga kutoka katika chama chake cha Likud.
Utafiti wa maoni ya raia kabla ya uchaguzi unaonyesha kuwa Saar anamkaribia sana Netanyahu kwa umaarufu miongoni mwa wapiga kura.
Saa kadhaa kabla ya muda wa mwisho kumalizika, Netanyahu ambaye ni kiongozi wa vuguvugu la mrengo wa kulia la chama cha Likud, na mpinzani wake wa kisiasa Benny Gantz kutoka vuguvugu la mrengo wa kati la Blue na nyeupe, walilaumiana kila upande ukiutuhumu mwingine kusababisha mzozo huo.