Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha 5.9 Jumatano usiku limetikisa baadhi ya maeneo ya Tanzania hususani ukanda wa pwani na kishindo chake Kufika mpaka katika baadhi ya maeneo ya nchi jirani ya Kenya.
Kwa mujibu wa taasisi ya uchunguzi wa jiolojia ya Marekani, 'US Geological Survey (USGS)', kitovu cha tetemeko hilo ilikuwa katika eneo lililopo kilomita 66 mashariki mwa mji mdogo wa Vikindu, Mkoani Pwani.
Tetemeko hilo lilipiga katika kina cha kilomita 15.5 (maili 9.6), lililotokea jijini Dar Es Salaam eneo linalojulikana kama jiji kuu la biashara nchini.
Mpaka sasa hakuna uharibifu wowote ulioripotiwa baada ya tetemeko hilo.
Tetemeko hilo imekuja siku chache baada ya wakazi wanaoishi pembezoni mwa ziwa Baringo nchini Kenya kuripotiwa kuwa na tetemeko baada ya kiwango cha maji kujaa kwa sababu ya mvua zinazoendelea.