Wafanyabiashara wametakiwa kuendesha biashara zao kwa uadilifu na huruma na kamwe wasitumie uwepo wa janga la Covid-19 kuwawekea mazingira magumu wananchi kwa kuwauzia bidhaa kwa bei kubwa hasa kipindi cha mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ameyasema hayo leo katika risala ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, ikiwa ni utaratibu wake aliuoweka unapokaribia mwezi huo Mtukufu kila mwaka.
Alhaj Dk. Shein amewaeleza wananchi kuwa mwaka huu wa 2020 mwezi Mtukufu wa Ramadhani unakaribishwa huku kukiwa na mtihani wa maradhi yanayosababishwa na virusi vya Korona vinavyojulikana kwa jina la COVID 19.
Rais Dk. Shein amewagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Masheha wahakikishe kwamba katika maeneo yao ya utawala wanavidhibiti vitendo vyote vinavyoweza kuathiri juhudi na mipango ya Serikali katika kupambana na maradhi hayo ikiwemo mikusanyiko ya watu.
Aidha, Alhaj Dk. Shein aliwanasihi wananchi wote wasisikilize taarifa zisizo rasmi wanazozitoa watu wasiohusika ambao hawana mamlaka ya Kiserikali ya kutangaza taarifa za Serikali.
Rais Shein amewatakia wananchi wote kheri na Baraka za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.