Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio la kusitisha mapigano kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa mgogoro nchini Libya, na kuzitaka pande zote husika kufikia makubaliano ya kudumu.
Mwezi Januari mwaka huu pande zinazokinzana nchini Libya zilifikia mkataba wa kusitisha mapigano, lakini mkataba huo mpaka sasa bado unalegalega kutokana na kuwa mapigano yamekuwa yakiendelea na kila upande ukishutumu upande mwingine kukiuka mkataba huo.
Azimio hilo limepitishwa baada ya mazungumzo yaliyodumu zaidi ya wiki tatu, huku kukionekana mgawanyiko wa kimataifa unaoendelea licha ya kuonyesha umoja wao katika mkutano uliofanyika kwenye mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, Januari 19 mwaka huu.
Mkutano huo ambao rais wa Urusi na Uturuki walishiriki kila mmoja alikuwa akionyesha kuunga mkono kambi moja hasimu iliyopo nchini Libya.
Azimio hilo ambalo bado halijafikiwa linataka kuwepo kwa makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano nchini Libya, kabla ya yote na bila masharti.
Urusi inashutumiwa kwa miezi kadhaa kuunga mkono usafirishaji wa maelfu ya mamluki wa kundi la Wagner, linalodaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na ikulu ya rais wa Urusi, kwenda nchini Libya kumsaidia Khalifa Haftar ambaye amekuwa akitafuta kuudhibiti mji wa Tripoli tangu Aprili 4, 2019.
Mwisho.