Star Tv

Walemavu wa Ngozi wanaoishi wilayani Monduli mkoani Arusha wapo hatarini kupata saratani ya Ngozi kutokana na kukosa mafuta maalumu yanayowasaidia kupunguza mionzi ya jua kutokana na kushindwa kumudu gharama za mafuta hayo.

 

Wakizungumza  katika kikao maalumu cha walemavu , Mathayo Lengasha na Leah Alex ambao ni mlemavu wa ngozi  wamesema kuwa wamekua wakisumbuliwa na saratani ya ngozi huku wakiomba serikali kuwapatia mafuta ya ngozi na bima ili waweze kutibiwa.

 

Mwenyekiti wa Shirikikisho la Vyama vya Walemavu katika Wilaya ya Monduli  Dorah Msuya amesema kuwa licha ya serikali kutoa maelekezo ya walemavu kutibiwa bila malipo bado ahadi hiyo haitekelezwi hivyo ameitaka serikali kutoa bima kwa walemavu..

 

Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Monduli Henrich Laizer  pamoja na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Monduli  ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara Noelia Myonga wamesema kuwa serikali itaendelea kuhakikisha kuwa walemavu wanapata haki zao ikiwemo ya matibabu kupitia sera na sheria mbalimbali zilizopo nchini....

 

Wilaya ya Monduli inakadiriwa kuwa na watu wenye ulemavu 672 ambao ni walemavu wa viungo, walemavu wa ngozi pamoja na walemavu wa akili.

 

Mwisho

Copyright © 2020 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.