Star Tv

 Uongozi wa Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza umepiga marufuku ibada zinazoendeshwa na kiongozi wa kanisa la  “Mfalme Zumaridi” lililoko mtaa wa Iseni kata ya Butimba hadi hapo Serikali itakapojiridhisha kuwa ibada hazikinzani na sheria za nchi.

 Agizo la kupiga marufuku limetolewa na Mkuu wa  Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza Daktari Philis Nyimbi akiwa ameongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo katika eneo la kanisa hilo. 

Daktari Nyimbi ametoa maelekezo kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha zinatumia vyema madaraka waliyopewa ya kusajili vyama vya kijamii kujiridhisha na utendaji kazi wa kanisa hilo  ili kuondoa sintofahamu yakufungiwa kwa kanisa hilo.

Baadhi ya wakazi wa maeneo hayo ambao wameshuhudia tukio hilo wameelezea kuhusu namna kiongozi huyo anavyoendesha ibada katika kanisa hilo huku wakiishukuru serikali kwa uamuzi  huo  ambapo baadhi yao wamesema kiongozi wakanisa hilo hatumii biblia, na pia anawakwaza

 “Mimi nimeishukuru serikali kwa kuweza kufunga huduma za hili kanisa, maana hata biblia hatumii wakati wa ibada na pia anatukwaza kwa kujiita Mungu wa Zumaridi , yeye ni mfalme”.

Pamoja na kiongozi wa Kanisa hilo Zumaridi kuwepo katika viwanja vya kanisa hilo na kuupokea ugeni wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Nyamagana hakuweza kuelezea kuhusu maamuzi ya serikali ya kupiga marufuku ibada na shughuli za kanisa hilo  ambalo limehudumu katika eneo hilo kwa muda wa miaka saba.

                   

                                                                                  Mwisho

                                                                              **********

Latest News


Social Media

Copyright © 2019 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.