KESI ZA UHUJUMU UCHUMI; Washtakiwa waanza kukiri makosa Washtakiwa watano wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi akiwemo wakili, Dk Ringo Tenga wamemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuomba kukiri makosa yao, ambapo wanadaiwa kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya bilioni nane Wakili wa washtakiwa hao, Byrson Shayo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Dk Ringo ambaye ni Mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni ya Mawasiliano ya Six Telecoms Limited na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwemo la kutakatisha fedha na kuisababishia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22. Mbali na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Mfanyabiashara na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms. Katika kesi ya msingi, Dk Ringo na wenzake wanadaiwa kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14, 2016 Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola za Marekani 0.25 kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida. Pia, katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya TCRA kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato. Vile vile ,washitakiwa hao wanadaiwa kuisababishia TCRA hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22. sawa na bilioni nane wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashtaka yaliyotangulia.