Star Tv

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 25 Juni, 2019 amezindua ghala na mitambo ya gesi ya mitungi inayotumika kupikia (Liquefied Petroleum Gas – LPG) inayomilikiwa na kampuni ya Watanzania iitwayo Taifa Gas Tanzania Limited katika Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taifa Gas Tanzania Limited Bw. Hamisi Ramadhani ameeleza kuwa uwekezaji mkubwa wa upanuzi wa ghala na mitambo ya gesi iliyopo Kigamboni umefanyika kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2018 ambapo umeongeza uwezo wake kutoka tani 1,650 hadi kufikia tani 7,650.

Uwekezaji huu umekwenda sambamba na ujenzi wa maghala na mitambo ya gesi katika Mikoa 20 hapa nchini kwa gharama ya shilingi Bilioni 150 na hivyo kuifanya Taifa Gas Tanzania Limited kuwa kampuni kubwa zaidi ya uwekezaji kwa idadi ya mitambo na kwa ukubwa wa ghala lenye mitambo ya kisasa kuliko yote Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Bw. Hamisi Ramadhani ameongeza kuwa uwekezaji huu umezalisha ajira za moja kwa moja 260 na zisizo za moja kwa moja 3,500 na kwamba pamoja na kuuza Tanzania kampuni hiyo inasambaza gesi katika nchini za Uganda, Rwanda, Burundi, DRC na Sudani Kusini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa Gas Tanzania Limited Bw. Rostam Azizi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuweka na kusimamia mazingira yenye usawa kwa wafanyabiashara na wawekezaji wote na kwamba kutokana na mazingira mazuri ya kufanyia biashara anatarajia kuongeza uwekezaji wa miradi mingine yenye thamani ya shilingi Bilioni 500 katika miaka 3 ijayo.

Msimamo wako thabiti dhidi ya matendo ya zamani ya ujanjaujanja katika biashara na uwekezaji, na ukwepaji wa kodi, ndivyo ambavyo leo hii vimetufanya baadhi yetu ambao kwa miaka tuliamua kuwekeza mitaji nje ya Tanzania, kupata moyo wa kuanza tena kurejesha mitaji hapa nyumbani” amesisitiza Bw. Rostam Azizi huku akitoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kutambua kuwa milango ya uwekezaji Tanzania iko wazi kwa uwekezaji madhari wanafuata sheria, taratibu na kanuni za nchi.

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani ameeleza kuwa kufuatia juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali kuanzia mwaka 2015 hadi sasa sekta ya nishati imepata mafanikio makubwa ikiwemo kuongezeka kwa Watanzania wanaotumia gesi ya kupikia kutoka Milioni 1 hadi Milioni 2.5, kuongezeka kwa uwezo wa nchi kupokea gesi kutoka tani 220,000 hadi tani 617,000 (ongezeko la asilimia 240), kampuni 8 za gesi ya kupikia kuajiri Watanzania 12,000 na uzalishaji wa umeme kuongezeka kutoka megawati 1,280 hadi kufikia megawati 1,601.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza kampuni ya Taifa Gas Tanzania Limited kwa uwekezaji huo na Wizara ya Nishati kwa kusimamia vizuri sekta ya nishati nchini ikiwemo kuongeza upatikanaji wa gesi ya kupikia kwa Watanzania, kuongeza usambazaji wa umeme kutoka vijiji 2,018 mwaka 2015 hadi kufikia vijiji 7,318 hivi sasa na kwa kuhakikisha matatizo ya kukatika umeme yaliyokuwepo awali yanapungua kwa kiasi kikubwa.

Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia miradi mikubwa ikiwemo miradi ya Mto Rufiji na Mto Ruhuji Mkoani Njombe ili kufikia megawati 5,000 zitakazowezesha kupunguza bei ya umeme na kukuza viwanda.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza sekta binafsi kwa uwekezaji uliofanywa katika sekta ya gesi ulioongeza uzalishaji wa gesi ya kupikia kutoka tani 17,000 mwaka 2015 hadi kufikia tani 92,500 hivi sasa na amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wengine wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza hapa nchi kwa kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao.

Ametoa wito kwa Taifa Gas Tanzania Limited na wawekezaji wengine wa sekta ya gesi kupanua huduma zao hadi vijijini ili Watanzania waondokane na matumizi ya mkaa na kuni katika kupikia na badala yake watumie gesi.

“Uwekezaji huu uliofanywa na Taifa Gas Tanzania Limited ni uthibitisho kuwa Serikali inapenda sekta binafsi, tunataka wawekezaji wa kweli sio maneno maneno, na wewe Rostam Azizi kama kuna wawekezaji huko walete, na umeniambia kiwanda chako cha ngozi kilichopo Morogoro kitakuwa tayari baada ya miezi 3, nitakuja” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu changamoto mbalimbali za Wilaya ya Kigamboni ikiwemo mradi mkubwa wa nyumba zilizojengwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF uitwao Dege, Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kwamba mradi huo umezingirwa na ufisadi, Serikali inasubiri Mamlaka husika ikiwemo NSSF na wananchi kutoa maoni ya nini kifanyike.

Sherehe za uzinduzi wa ghala na mitambo ya gesi ya Taifa Gas Tanzania Limited zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa, wawekezaji mbalimbali na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Makonda.

 CHANZO: Ikulu Mawasiliano. 

Latest News

Mgogoro wa Maji unatishia Amani Duniani, inasema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa...
21 Mar 2024 14:18 - Kisali Shombe

Siku ya Maji Duniani ambayo inafanyika tarehe 22 Machi ikiwa na kaulimbiu: 'Maji kwa Ustawi na Amani. Ambapo maji ni moj [ ... ]

Matarajio katika mkutano wa BRICS nchini Afrika Kusini, Jumanne tarehe 22/2023
21 Aug 2023 12:14 - Kisali Shombe

Mkutano huo ambao utafanyikia Johannesburg nchini Afrika Kusini siku ya Jumanne, tarehe 22 Agosti 2023, unatarajiwa kuhu [ ... ]

Rais Ramaphosa Kuwa Mwenyeji wa Rais Xi Jinping wa China
21 Aug 2023 11:11 - Kisali Shombe

Rais Cyril Ramaphosa Jumanne ya tarehe 22 Agosti 2023, atakuwa mwenyeji wa Mheshimiwa Rais Xi Jinping wa China katika Zi [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2024 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.