Shirika la ugavi wa umeme TANESCO Mkoani Kagera limewaonya wajasiriamali wanaotumia umeme kwa njia za wizi ili kuutumia katika mitambo yao ya kutega senene hususani nyakati za usiku.
Oparesheni ya kushtukiza iliyofanywa na maafisa wa TANESCO katika kijiji cha Ngarama kata ya Katoro wilayani Bukoba imebaini asilimia kubwa ya nyumba katika kijiji hicho kuunganishiwa umeme kwa njia za wizi pasi na kufuata utaratibu. Afisa Usalama wa TANESCO mkoani Kagera Stephen Maganga amesema umeme unaoibiwa ni ule unaotumika katika mitambo ya kutegea senene nyakati za usiku na kuwataka wananchi hao kuacha la sivyo hatua kali za kisheria zitachuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuondoa nguzo zote za umeme katika kijiji hicho.
Pamoja na wakazi wengi wa kijiji hicho kukimbia mara baada ya kusikia uwepo wa oparesheni hiyo,Mwenyekiti wa serikali ya kijiji Abdulkarim Twaha amelitaka shirika hilo kufanya oparesheni za mara kwa mara pamoja na kuchunguza baadhi ya watumishi wa shirika hilo wanaoshirikiana na vishoka kufanya hujuma hizo maafisa hao walilazimika kufanya kazi ya ziada ya kuwaweka chini ya ulinzi baadhi ya wakazi waliobainika kushiriki katika hujuma hizo.