Star Tv

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Machi, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Mhe. Sheikh Mohammed bin Abdulrahman J.A. Al Thani, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao wamezungumzia uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Qatar na dhamira yao ya kuhakikisha uhusiano na ushirikiano huo unaendelezwa na kukuzwa zaidi hususani katika masuala ya uwekezaji katika gesi, madini, utalii na miundombinu ya barabara, bandari, nishati, reli na huduma za kijamii.

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Sheikh Mohammed kwa kuja kwake hapa nchini pamoja ujumbe wa wawekezaji wenye dhamira ya kuwekeza nchini Tanzania na amemuomba ampelekee salamu za shukrani kwa Mtawala wa Taifa la Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani kwa kuendeleza uhusiano na Tanzania.

Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania inazo fursa nyingi za uwekezaji zikiwemo uchakataji wa gesi, madini, utalii na usafiri wa anga hivyo amemuomba Sheikh Mohammed kuwahamasisha wafanyabiashara wa Qatar kushirikiana na Tanzania kuwekeza katika maeneo hayo.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameiomba Qatar kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo uzalishaji wa nishati ya umeme, ujenzi wa reli, barabara na madaraja na pia amemualika Mtawala wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani kufanya ziara hapa Tanzania.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed amemshukuru Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake kwa kuendelea kushirikiana na Qatar katika masuala mbalimbali na kubainisha kuwa Qatar inathamini uhusiano huo.

Sheikh Mohammed ameahidi kuwa Qatar ipo tayari kufanyia kazi maombi yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli na pia kuzileta kampuni za nchi hiyo kuja kuwekeza katika maeneo yenye fursa zenye manufaa kwa pande zote mbili.

Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema baada ya kukutana na Mhe. Rais Magufuli, yeye na Sheikh Mohammed watakua na mazungumzo ya kina kuhusu maeneo ya ushirikiano.

Mazungumzo ya viongozi hao yamehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Qatar Mhe. Fatma Rajab na Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe. Abdullah Jassim Mohammed Al Medadi.

Chanzo; Ikulu

 

Latest News

Mwanafunzi apoteza maisha, baada ya kutumbukia kisimani.
17 Sep 2019 10:27 - Kisali Shombe

Mwanafunzi¬†mmoja Matutu Mashini (7) aliyekuwa anasoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Salama A, iliyoko katika  [ ... ]

Rais Magufuli atengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya W...
17 Sep 2019 10:02 - Kisali Shombe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mko [ ... ]

Nape Nnauye akutana na Mhe. Rais Magufuli, amuomba radhi.
10 Sep 2019 11:44 - Kisali Shombe

Mbunge wa Jimbo la Mtama Mkoani Lindi, Mhe. Nape Nnauye amekutana na kumuomba radhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanza [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2019 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.