Star Tv

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali ya nchi hiyo haiwezi kutoa mikopo ya kimasomo kwa wanafunzi wote wa vyuo vikuu nchini humo.

Kiongozi huyo alisema serikali yake imekuwa ikiongeza fedha za mikopo na kuwakopesha wanafunzi wengi zaidi lakini akasisitiza kuwa sasa haitaweza kutoa mikopo kwa wanafunzi wote wa vyuo vikuu.

"Nataka niwahakikishie Serikali ya Awamu ya Tano inawapenda wanafunzi wa vyuo vikuu, lakini lazima niwaambie ukweli Serikali haiwezi kutoa mikopo kwa wanafunzi wote" alisema.

Dkt Magufuli alisema hayo alipokutana na wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kilichopo katika Manispaa ya Iringa ambapo alisikiliza kero zao mbalimbali zikiwemo zinazohusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na mazingira ya kusomea, kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu.

Rais Magufuli alisema utoaji wa mikopo ya elimu ya juu ni lazima ufuate taratibu pamoja na historia ya familia.

Alidokeza kwamba watakaopewa kipaumbele ni wale wanaosomea udaktari, ualimu na uhandisi.

"Hili suala la mikopo lina changamoto, ndiyo maana tunapotoa mikopo tunaangalia historia ya mtu, ndiyo maana mtoto wangu hapati mkopo," alisema kwa mujibu wa gazeti la kibinafsi la Mwananchi.

"Huwezi kumsomesha mtoto shule ya msingi ya binafsi, halafu baadaye aje aombe mkopo.

Hao waliokusomesha wapo wapi? Na kama hawapo tutataka uambatanishe nyaraka kuonyesha hawapo.

" Rais huyo alitania kwamba wanawe walijaribu kutumia ujanja wa kutumia jina la mama yao kupata mikopo lakini hawakufanikiwa. "Hawa majamaa wajanja sana, tulijaribu kutumia jina la mama yao lakini bado wakawagundua," alisema.

Mwishoni mwa mwaka jana, serikali ya Tanzania iliidhinisha Sh427 bilioni za mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2017/18, lakini viongozi wa wanafunzi walilalamika kuwa bajeti hiyo ilikuwa ndogo ukilinganisha na mahitaji.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya viongozi wa wanafunzi walisema bajeti hiyo imekuwa ikizidi kupungua licha ya wanafunzi kuongezeka.

Mkurugenzi wa haki za wanafunzi wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo aliambia gazeti la Mwananchi wakati huo kwamba bajeti hiyo imekuwa ikizidi kupungua licha ya wanafunzi kuongezeka.

Mwaka 2016/17 serikali ilitenga Sh483 bilioni kwa wanafunzi 120,000 za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. "Cha kushangaza mwaka wa masomo 2017/18 wanafunzi wameongezeka na kufikia 122,000, lakini badala ya fedha za mkopo kuongezeka zimepungua na kuwa Sh427 bilioni waombaji wakiwa 61,000 na Serikali imesema itawapa 30,000 pekee," alisema.

Lakini naibu waziri wa Elimu, William Ole Nasha alisema Serikali imetenga fedha hizo kulingana na maombi ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).

Alisema: "Kuna vigezo ambavyo vimewekwa na kulingana na vigezo hivyo bodi imejiridhisha fedha hizo zinatosha, bodi ingeomba halafu Serikali ingepunguza lawama hizo zingekuwa na tija.

"Alieleza kuwa vigezo vinavyotumika ni ngumu kubaini ukweli wake kwa sababu si kila anayeishi katika familia bora ana uwezo.

Mkurugenzi wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alinukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema changamoto iliyopo ni baadhi ya wanafunzi na wazazi kuamini hata kama wana uwezo ni lazima wapate mkopo.

"Siyo kweli kwamba wanafunzi Tanzania nzima hawana uwezo wa kumudu gharama za kusoma vyuoni, ila imejengeka dhana kuwa wakifika chuo kikuu lazima walipiwe na Serikali," alisema.

Miongoni mwa changamoto zinazokabili mpango wa utoaji mikopo kwa wanafunzi Tanzania, kwa mujibu wa serikali, ni baadhi ya wanafunzi walionufaika kutolipa pesa hizo.

Mapema mwaka huu Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wiki ijayo ilitangaza kuanza kuwasaka jumla ya wanufaika 119,497 nchini kote ambao wamekiuka sheria iliyoanzisha Bodi hiyo.

Wanufaika hao walidaiwa kutoanza kurejesha mikopo yenye thamani ya TZS 285 bilioni waliyokopeshwa tangu mwaka 1994/1995 na mikopo yao.

Kwa hisani ya BBC

Latest News

Mgogoro wa Maji unatishia Amani Duniani, inasema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa...
21 Mar 2024 14:18 - Kisali Shombe

Siku ya Maji Duniani ambayo inafanyika tarehe 22 Machi ikiwa na kaulimbiu: 'Maji kwa Ustawi na Amani. Ambapo maji ni moj [ ... ]

Matarajio katika mkutano wa BRICS nchini Afrika Kusini, Jumanne tarehe 22/2023
21 Aug 2023 12:14 - Kisali Shombe

Mkutano huo ambao utafanyikia Johannesburg nchini Afrika Kusini siku ya Jumanne, tarehe 22 Agosti 2023, unatarajiwa kuhu [ ... ]

Rais Ramaphosa Kuwa Mwenyeji wa Rais Xi Jinping wa China
21 Aug 2023 11:11 - Kisali Shombe

Rais Cyril Ramaphosa Jumanne ya tarehe 22 Agosti 2023, atakuwa mwenyeji wa Mheshimiwa Rais Xi Jinping wa China katika Zi [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2024 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.