Star Tv

Mtanzania Rashid Charles Mberesero aliyehukumiwa kifungo cha maisha mwaka 2019 baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki shambulizi la kigaidi mnamo 2015, amejitia kitanzi katika gereza la Kamiti.

Msemaji wa idara ya magereza Kennedy Aluda jana Jumapili Nov 29,2020 alivieleza vyombo vya habari nchini Kenya kwamba, Bwana Mberesero alipatikana amejinyonga gereza namba 24 kwenye jumba la H.

“Alitumia blanketi kama kamba na kujinyonga. Mwili wake ulipatika ukining’inia kupitia dirishani ukiwa na blanketi shingoni”- alisema Bwana Aluda.

Aidha, Msemaji idara ya Gereza amesema kuwa uchunguzi tayari umeanzishwa kubaini kilichomsukuma Mberesero kujitoa uhai, Hata hivyo, marehemu alikuwa na tatizo la kiakili na alikuwa akipokea matibabu mara kwa mara.

Taarifa ndani ya gereza hilo zilisema marehemu alidungwa sindano Alhamisi kabla ya kujiua siku iliyofuata saa nane mchana, lakini pia upasuaji wa maiti utafanywa kubaini chanzo kamili cha kifo chake.

“Uchunguzi huo hata hivyo lazima uhusishe familia yake iliyoko nchini Tanzania”- aliongeza Bw Aluda.

Bw Mberesero alikuwa akitumikia kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kushambulia Chuo cha Garissa mnamo Aprili 2015. Shambulizi hilo lilisababisha vifo vya watu 150 ambao wengi walikuwa wanafunzi huku wengine 100 wakijeruhiwa.

Polisi walisema Jumapili walipokea ripoti katika kituo cha polisi cha Kahawa Magharibi kutoka kwa afisa anayehusika na masuala ya usalama katika gereza la Kamiti kwamba kuna mahabusu aliyekuwa amejinyonga gerezani saa moja kasoro dakika 10 jioni.

“Maafisa wa polisi walitembelea gereza hilo nambari 24 kwenye jengo la H na wakapata mwili wa Rashid Charles Mberesero, raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 25 ukiwa umening’inia na umefungwa kwa blanketi shingoni na kwenye chuma cha dirisha”- ilibainisha ripoti kwenye kituo hicho cha polisi.

Marehemu alipatikana na hatia ya kupanga njama ya kutekeleza mashambulizi ya kigaidi na mahakama moja ya Nairobi mwaka 2019.

Alihukumiwa maisha lakini wenzake Mohamed Abdi Abikar na Hassan Aden Hassan wakapewa hukumu nyingine, Ambapo rekodi za mawasiliano kwenye simu na maandishi yalithibitisha watatu hao walihusika na shambulizi hilo la kigaidi.

 

Latest News

BIDEN KUSAINI MAAGIZO 12 YA RAIS.
17 Jan 2021 07:08 - Grace Melleor

Rais mteule wa Marekani Joe Biden atatia saini maagizo 12 ya rais siku ya kuapishwa kwake kuwa rais wiki ijayo ili kushu [ ... ]

MUSEVENI AWAONYA WAFUASI WA UPINZANI KUTOZUA GHASIA.
17 Jan 2021 06:10 - Grace Melleor

Rais wa muda mrefu nchini Uganda Yoweri Museveni jana Jumamosi ameonya kuwa vikosi vya usalama vitatumia nguvu kuzima ju [ ... ]

WATU WAWILI WANUSURIKA KUAWA NA WANANCHI WENYE HASIRA KALI.
17 Jan 2021 05:42 - Grace Melleor

Watu wawili wakazi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara wamenusurika kuawa na wananchi wenye hasira kali kutoka kwa vijana  [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2021 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.