Kundi la Islamic State (IS), kupitia shirika lake la propaganda AMAQ, limekiri kuhusika na shambulio lililogharimu maisha ya afisa mmoja wa kikosi cha ulinzi wa taifa jana Jumapili huko Sousse, mji wa kitalii Mashariki mwa Tunisia.
Jumapili mapema asubuhi, watu waliokuwa kwenye gari waliwavizia maafisa wa kikosi cha ulinzi wa taifa karibu na eneo lililo karibu na bandari ya Kantaoui, katika mji wa kitalii wa Sousse, kisha wakawashambulia kwa kisu, na kumuua mmoja wao na pia kumjeruhi vibaya mwingine.
Kundi la IS limetangaza kifo cha afisa mmoja wa vikosi vya usalama katika shambulio lililofanywa na "wapiganaji" wa kundi hilo, bila hata kutoa maelezo zaidi.
Wauaji watatu, ikiwa ni pamoja na ndugu wawili, waliuawa Jumapili asubuhi katika eneo hilo hilo na hawakuwa wanajulikana na mamlaka nchini Tunisia.
Watu saba pia walikamatwa kuhusiana na uchunguzi huo, ikiwa ni pamoja na mke wa mmoja wa washambuliaji, ndugu wawili na mtu mmoja anayeshukiwa kuwa msajili, kimebaini kikosi cha ulinzi wa taifa.
Shambulio hili jipya dhidi ya vikosi vya usalama, katika jiji ambalo moja ya mashambulizi mabaya ya kijihadi ambayo yaliikumba nchi hiyo mwaka 2015, lilitokea siku tatu baada ya serikali mpya kuapishwa, baada ya mvutano mkali wa kisiasa.